Saturday, January 19, 2013

Leo ndiyo ile siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu uwanja wa Mkwakwani...

Mshambuliaji mwenye mashuti makali kutoka nchini Brazil Gabriel Barbosa leo ataonyesha makali yake na kuwadhihirishia wapenzi wa soka Tanzania kuwa hajakuja Tanzania kuonyesha mavazi. Barbosa atakuwa Mbrazil wa kwanza kucheza soka katika ligi kuu ya Tanzania tangu nchi hii kupata uhuru. Na Coastal Union itaandika historia hiyo siku ya tarehe 26 katika uwanja wa Mkwakwani Tanga wakati itakapofungua dimba la mzunguko wa pili wa ligi kuu dhidi ya Mgambo FC ya Handeni Tanga.

Hiki ndicho kikosi namba moja kitakachoanza leo dhidi ya African Sports watani wa jadi wa siku nyingi wa Coastal Union. Kikosi hiki ndicho kilichoanza jana dhidi ya AFC ya Arusha katika mechi ya kujipima nguvu uwanja wa Mkwakwani ambapo AFC ilipigwa 1-0. Barbosa ni wa saba kutoka kulia yupo katikati ya Razack na Kibacha.

Siku ya leo saa kumi alasiri wapenzi wa soka mjini Tanga hawatakwenda kuangalia soka kama nilivyotangulia kusema jana, bali watakwenda kurudishia zile zama za kutambiana na kusema maneno ya kejeli kwa timu pinzani. Zamani ilikuwa ukijiita African Sports basi unaweza hata kunyimwa mke na baba ambae ni Coastal Union.

Watu walikubali kuzikwa baharini ili timu yake ishinde ama kufanya chochote ili kuhakikisha timu yake haifungwi na mpinzani.

Leo blog yako katika kukumbusha furaha hiyo itakuletea picha nyingi za ushabiki kuanzia mitaani kabla mechi wakati wa mechi na baada ya mechi. Lengo ni kukuletea burudani ileile ambayo wapenzi wa soka mjini Tanga wameipata.

Coastal Union
Tanga, Tanzania

No comments:

Post a Comment