Tuesday, February 12, 2013

Coastal Union leo wamefanya mazoezi ya nguvu chini ya mvua kali.. Bukoba.

 Hamad, Shengo na Nzara Ndaro wakivinjari mitaani katika mkoa wa Kagera, utasema wenyeji vile.


                             Gabriel Barbosa anasema yupo fit kwa game hatowaangusha vijana wa Tanga.
 
Ndugu zangu,

Timu ya Coastal union kama ilivyoelezwa jana iliingia mjini Bukoba majira ya saa kumi na mbili kasoro jioni ikitokea mjini Mwanza kwa usafiri binafsi. Mwanza kulikuwa na hali ya joto na baridi ya wastani, lakini Bukoba kuna baridi na mvua kidogo.

Leo asubuhi timu ilifanya mazoezi katika uwanja wa Kaitaba pembezoni mwa ziwa Victoria. Hali ya hewa ni baridi na mvua, timu imefanya mazoezi katika mvua kali.

Hii itasaidia kuwaweka imara kwa maana watazoea hali hii hata kesho wakati wa mechi kama kutanyesha mvua hawataona ajabu wala kuhisi tofauti.

Kitu tulichokutana nacho Bukoba ni mpira wa redioni, au kule kwetu tumezoea kuita mpira wa midomoni. Viongozi wa Kagera wanajitahidi sana kututisha ili mechi tuione ngumu, hatujafanyiwa hujuma zozote mpaka sasa wala roho mbaya lakini wanatumia redio zao kutoa vitisho.

Kwanza wanasema timu ya Kagera sugar imeunda kamati ya saidia Kagera Sugar ishinde, yaani iwe ni mbiu ya mkoa mzima wa Kagera kuhakikisha wanashinda mechi zote za nyumbani na ugenini.

Wanasema watahakikisha uwanja unajaa mashabiki wao ili washangilie kwa nguvu kuwapoteza malengo wachezaji wa wagosi wa kaya.

Hata hivyo blog hii ilizungumza na baadhi ya wenyeji ambao wamesema Kagera sugar haina wapenzi hapa Bukoba, haipendwi na wala hakuna mtu anaejishughulisha.

Malalamiko makubwa wanayoyatoa wenyeji wa Bukoba ni namna kiwanda cha sukari cha Kagera kilivyopandisha bei ya sukari katika mkoa huu ili pesa zinazopatikana zisaidie timu wanalipinga sana suala hilo.

Aidha viongozi wa Kagera Sugar wanaifananisha Coastal Union na JKT Mgambo, ati kwasababu waliwafunga mechi iliyopita tarehe 9 feb, lakini nawasikitikia sana kwa kufananisha mbingu na ardhi.

Kocha mkuu wa Coastal Union Hemed Morroco anasema “Sisi tumekuja kutafuta ushindi maneno yao hayatutishi, wachezaji wangu ni bora mara sabini ya wao, hivyo ninachotaka kukwambia usitishike na maneno yao.”

Nae mwyekiti wa timu Hemed Hilal ‘Aurora’ amesema hawezi kupoteza muda na pesa kutoka Tanga kuja Bukoba halafu warudi bila ushindi, hicho kitu hakiwezekani katu.

Coastal Union Wagosi wa kaya kesho watashuka dimbani katika uwanja wa Kaitaba Bukoba kumenyana na Kagera sugar katika mchezo wao wa nne kwenye ligi kuu Tanzania bara mzunguko wa pili.

Kagera sugar inashuka dimbani ikiwa na point 24 katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi wenye timu 14, wakati wagosi wa kaya wana point 27 katika nafasi ya nne. Wakishinda mchezo wa leo watakwea nafasi moja juu na kuwa nafasi ya tatu kitu wanachokililia kwa muda mrefu.

Mungu isaidie Coastal Union Mungu usaidie mkoa wa Tanga urudishe heshima yake ya soka iliyokuwa nayo kwa miaka mingi hata kabla ya uhuru kupatikana mwaka 1962.

COASTAL UNION
12,02,2013
Kagera,Tanzania

No comments:

Post a Comment