Sunday, February 3, 2013

Morroco anasema tunampumulia simba mgongoni kwa tofauti ya Point moja tu.....

                                Kocha mkuu wa Coastal Union wagosi wa kaya Hemed Morroco.


Na Mwandishi maalum

Timu ya Coastal Union kutoka mjini Tanga leo imetoa suluhu tasa dhidi ya wajelajela Prison ya Mbeya katika uwanja wa mkwakwani na kuendelea kubakia katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu chini ya wekundu wa msimbazi Simba inayoshikilia nafasi ya tatu.

Mchezo wa leo ulikuwa wa kukamiana kwani maafande wa Prison walitaka kurekebisha makosa baada ya kufungwa 3-1 katika mechi yao ya kwanza ya mzunguko wa pili dhidi ya Yanga  katika uwanja wa taifa Dar es Salaam, dakika za awali mchezaji wa Coastal Union Danny Lyanga aliipatia timu yake bao la kuongoza lakini refa akasema alikuwa ameotea ‘offside’.

Coastal Union ambayo langoni alikaa golikipa aliesajiliwa katika dirisha dogo kutoka mtibwa Sugar Shaaban Kado, wengine ni Ismail Suma, Othman Tamim, Bakari Kibacha, Philip Mugenzi, Jerry Santo, Lameck Dayton, Shango, Danny Lyanga, Suleiman Kassim Selembe na Mahundi.

Katika dakika za majeruhi kipindi cha pili kocha wa Coastal Union Hemed Morroco alifanya mabadiliko akamtoa Mahundi akaingia Mbrazil Gabriel Barbosa ambae amecheza kwa mara ya kwanza katika ligi kuu ya Tanzania Bara. Baadae akatoka Shango akaingia Castro Mumbala.

Mbrazil Barbosa ambae kwa kipindi kirefu alikuwa midomoni mwa mashabiki wa Coastal Union juu ya uwezo wake kisoka, leo alionyesha soka la hali ya juu katika dakika 15 za mwisho alizoingizwa. Alikosa magoli mengi lakini lile lililoamsha watu ni pale alipopga tick tack lakini golikipa wa Prison alikuwa imara na kumkosesha bao Barbosa.

Kwa matokeo hayo Coastal Union itaendelea kubakia nafasi ya nne ikiwa na point 26, chini ya Simba ambayo ina point 27 baada ya kutoka suluhu ya moja kwa moja leo dhidi ya JKT Ruvu katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Yanga wamebaki kileleni na point 33 ambao nao walitoka suluhu ya moja kwa moja dhidi ya Mtibwa Sugar jana kwenye uwanja wa Taifa jijini. Azam wao wapo nafasi ya pili wakiwa na point 30 baada ya kuwachabanga 3-1 Toto Africa katika uwanja wa Chamazi kwenye mchezo wao wa pili.

Ligi sasa imekuwa na upinzani mkali kwani timu nne za juu yaani Yanga, Azam, Simba na Coastal Union zinaonyesha upinzani mkubwa na macho ya watanzania wengi yamehamia katika timu hizo ingawa zipo timu kama Africa Lyon, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zinacheza mpira wa nguvu na wa kukamia.

Coastal Union itacheza tena mechi yake ya tatu tarehe 9 mwezi wa pili dhidi ya Toto Africa katika uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na watabaki hukohuko kanda ya ziwa wakisubiri mechi yao nyingine tarehe 13 mwezi wa pili mwaka huu dhidi ya Kagera Sugar katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Coastal Union
Dar es Salaam, Tanzania
3/2/2013



No comments:

Post a Comment