Huyu ndiye Ally Nassor 'Ufudu' aliyepachika bao la pekee kwenye mechi ya leo dhidi ya Oljoro. pembeni yake ni meneja na timu B, Abdulrahman Mwinjuma 'Ubinde'.
Mshambuliaji chipukizi wa Coastal Union chini ya miaka 20,
Ally Nassor ‘Ufudu’ ameanza kuwa gumzo jijini Arusha baada ya kupachika mabao
katika mechi mbuili mfululizo zilizochezwa jana na leo huku akiwa msumbufu kwa
mabeki wa timu pinzani.
Coastal Union wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya
maafande wa JKT Oljoro kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid kwenye
michuano ya vijana chini ya miaka 20 Rollingstone inayofanyika kwa mara ya 14 mfululizo
tangu ilivyoanzishwa mwaka 1999 na kituo cha kukuza vipaji jijini humo cha
Rollingsone Academy.
Wagosi walijipatia bao la kwanza na la pekee kwenye mechi ya
leo baada ya kutoka vichwa chini kwenye dakika 45 za mwanzo kutokana na timu
zote kucheza kwa kuviziana kwakuwa zinafahamiana aina ya uchezaji kwa kipindi
kirefu.
Kama kawaida yake kocha wa Wagosi wa kaya Bakari Shime huwa
anautumia vema muda wa mapumziko kwa kuwaelekeza wachezaji wake nini cha
kufanya, hivyo mnamo dakika ya 49 Ally Ufudu alipokea pasi murua kutoka kwa
Mohammed Issa ‘Banka’ na kumsukumia shuti kali golikipa wa Oljoro ambaye
alishindwa kujinyoosha na kuuangalia mpira ukitinga wavuni bila msaada wowote.
Baada ya hapo Oljoro walikasirika na kuelekeza mashambulizi
ya kasi langoni mwa Coastal Union lakini golikipa mwenye mbwembwe nyingi na
ujuzi wa hali ya juu Mansour Alawi Mansour aliwakatisha tama washambuliaji wa
maafande hao kwa kuzuia mashuti yao hafufu kwa mkono mmoja huku akisaidiwa na
mabeki wenye roho ngumu wa Coastal Union, Mwaita Saleh, Hussein Zolla na
nahodha wa kikosi cha ubingwa Nzara Ndaro.
Hata hivyo Ally Ufudu manusura awanyanyue katika benchi
viongozi wa Coastal Union baada ya kuwapangua mabeki wa Oljoro halafu akabaki
yeye na golikipa mnamo dakika ya 70 ya mchezo lakini kwa bahati mbaya akapata
kigugumizi cha miguu na kupaisha mpira ikawa ni goal kick.
Aidha, Kikosi kilichoanza leo ni 1. Mansour Alawi, 2.Mwaita
Saleh, 3.Hussein Amri ‘Zolla’, 4.Nzara Ndaro (captain), 5.Yusuf Chuma ‘Croach’,
6.Aziz Fatawi, 7.Mohammes Issa ‘Banka’, 8.Behewa Sembwana, 9.Mohammed Hassan,
10. Alli Nassor ‘Ufudu’, 11.Ayoub Semtawa.
Siku ya jana vijana walicheza na Young Life wakashinda 3-0 ambapo
Ally Ufudu alipachika mabao mawili peke yake huku Behewa Sembwana akifunga bao
moja hivyo mpaka sasa wana point 6 na taarifa zinasema keshokutwa watashuka
dimbani kukamilisha hatua ya makundi dhidi ya Testimonial Academy pia kutoka
Arusha.
COASTAL UNION
9 Julai, 2013
No comments:
Post a Comment