Saturday, July 6, 2013

Timu ya vijana chini ya miaka 20 Coastal Union kutua Arusha leo.

Kocha Bakari Shime akihakikisha vijana wake wanakuwa na misuli imara katika viwanja vya Popatlal jijini Tanga.

Hatimaye timu ndogo ya Coastal Union imethibitisha ushiriki wa michuano ya vijana kutoka nchi za afrika Mashariki na kati inayofanyika jijini Arusha kuanzia leo.
Akizungumza kwa njia ya simu wakati wa kuanza safari jijini Tanga kuelekea Arusha asubuhi hii meneja wa timu hiyo Abdulrahman Mwinjuma ‘Ubinde’ amesema tayari kocha amejipanga vizuri kuhakikisha wanachukua ubingwa kwenye michuano hiyo ya Rolling Stone ambapo mwaka jana walifika hatua ya fainali ilipofanyika jijini Bujumbura nchini Burundi wakatolewa na timu kutoka Congo.
“Mwaka huu tumedhamiria, viongozi wametukabidhi dhamana na tutahakikisha tunaleta furaha kwenye klabu yetu ambapo kwa kipindi kirefu tumekuwa na ukame wa vikombe, hivyo tunaondoka kuelekea Arusha tukiwa na akili moja tu ya ubingwa,” alisema.
Hata hivyo timu B imechelewa kuelekea Arusha kutokana na kocha Bakari Shime kuwa na wakati mgumu wa kuchagua kikosi cha kuelekea nacho Arusha kwani kulikuwa na vijana takriban 50 ambao wote walikuwa katika majaribio hivyo kumpa wakati mgumu Shime.
Aidha leo ndiyo ufunguzi ambapo timu ya vijana Eagle FC nayo kutoka Tanga, itashuka dimbani katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Azam FC.
Kwa mujibu wa Ubinde watakapofika ndipo watakapojua kuhusu ratiba ya michuano hiyo ambayo itaisha Julai 19 mwaka huu.
COASTAL UNION
6 Julai, 2013

No comments:

Post a Comment