Ukisikia kivumbi na mwenzake jasho ndo hiki. Taraa. |
Yooote tisa kumi mabeki wa caostal Union leo walikuwa imara sana, hapa Hamad Juma 'Basmat' akitafuta mbinu za kumtoka mchezaji wa Azam.
Leo Ally Ufudu alifunikwa kabisa, Azam waliambiwa wamkabe sana kijana huyu. Hapa akituliza mpira huku mchezaji wa Azam akijiandaa kuenda kuuharibu.
Baada ya dakika 90 kuisha kocha Bakari Shime akipanga mashambulizi upya kujiandaa na dakika 30 za nyongeza.
Benchi la Coastal Union hili baada ya abdul Ubinde kupewa kadi nyekundu.
Bakari Mwaita akikimbia na mpira huku mchezaji wa Azam akiumezea mate. |
Ayoub Semtawa akipewa kadi nyekundu na mwamuzi wa leo.
Mchezaji wa Azam FC akipewa kadi nyekundu baada ya kumchezea madhambi Ally Ufudu. |
Mansour Alawi akishangaa mpira unaingia wavuni hii ni penati ya tano na ya mwisho tumelala kwa penati 4-5.
Coastal Union chini ya miaka 20 wameaga michuano ya
Rollingstone katika hatua ya nusu fainali baada ya kutolewa na Azam FC kwa
mikwaju ya penati 4-5 kwenye uwanja wa General Tyre asubuhi hii.
Mechi ya leo iliyokwenda mpaka dakika 120 baada ya dakika 90
za kaiwaida kuisha kwa suluhu ya bila kufungana, zikaongezwa dakika 30 lakini
hazikusaidia kubadili matokeo kila timu ilishindwa kuchungulia nyavu za
mwenzake.
Aliyeharibu furaha za wagosi wa kaya ni Mohammed Hassan
aliyeingia kipindi cha pili kukosa penati ya kwanza kwa kupaisha mwamba wa juu
ndipo Azam wakapata nguvu na kutumbukiza wavuni penati zote tano ingawa Coastal
Union walifanikiwa kutumbukiza penati nne zilizobaki lakini hazikufua dafu.
Mchezo ulikuwa wa kukamiana lakini mashabiki wa Coastal
Union wakati wote walikuwa wakitupa lawama kwa mwamuzi wa kati na wanyoosha
vibendera kwa dhana kuwa wamenunuliwa na Azam FC baada ya kitendo cha
kustaajabisha kabla ya mchezo kuanza Bus la Azam lilipokuwa likiingia uwanja wa
General Tyre waamuzi nao walionekana wakishuka pamoja na wachezaji wa Azam.
Katika dakika 45 za mwanzo Coastal Union walikosa mabao
takriban matatu baada ya mchungulia nyavu maarufu Ally Nassor Ufudi kupata
nafasi tatu akiwa yeye na golikipa lakini alipaisha juu. Azam nao walikuwa
wakiliandama lango la Coastal Union lakini mabeki imara wa wagosi walimhami
Mansor Alawi aliyekuwa langoni mwa Wagosi.
Baada ya maamuzi ya mwamuzi wa kati Emmanuel Mwandembwa,
kuwa mabaya kupita kiasi meneja wa Coastal Union, Abdulrahman Ubinde aliingilia
kati na kuzungumza na mkutugenzi wa michuano aliyetambulika kwa jina moja la
Wilbroad lakini Wilbroad alimweleza mwamuzi amuondoe jukwaani Ubinde kwa
maelezo kuwa anafanya vurugu.
Kipindi cha pili mpira ulibadilika ambapo Azam walianza kwa
kasi na kucheza madhambi ya kusudi, katika dakika ya 70 nahodha wa Coastal
Union Nzara Ndaro almanusra apewe kadi nyekundu kwa kutaka kupigana na mchezaji
wa Azam kutokana na madhambi ya maudhi.
Dakika kumi kabla ya mchezo kuisha Ayoub Semtawa alionyeshwa kadi ya njano,
kwakuwa alikuwa na kadi nyingine hivyo ikawa ni nyekundu.
Katika dakika 30 za nyingeza mpira ulikuwa wa kukamiana na
umakini wa hali ya juu, lakini mpaka nusu ya kwanza inaisha hakuna aliyeona
lango la mwenzake. Ndipo katika dakika 15 za pili mwamuzi akamuonyesha kadi
nyekundu mchezaji wa Azam baada ya kumchezea madhambi Ally Ufudu.
Katika penati alianza Mohammed Hassan akakosa, akafuata
Hammad Juma, Mohammed Hassan Omary, Bakari Mwaita na Mwaita Salehe wote
wakapata. Lakini kulitokea sintofahamu baada ya Mwaita Salehe kupiga penati na
kukosa lakini mwamuzi akasema irudiwe baada ya golikipa wa Azam FC kutoka kabla
penati haijapigwa, ndipo akapata lakini haikusaidia kitu kwani mchezaji wa Azam
aliyepangwa kumalizia penati alipata.
Kwa matokeo hayo Azam FC watacheza fainali na Eagle Rangers
ya Tanga, huku mshindi wa tatu Coastal Union watashuka dimbani dhidi ya JKT
Oljoro waliofungwa mabao 2-1 na Eagle Rangers.
Hata hivyo baada ya mpira kuisha wachezaji wa Coastal Union
waliingia kwenye bus lao kimya kimya ila wachezaji wa Azam FC waliokuwa
wamejawa furaha ya ushindi walikuja kwenye Bus la Coastal Union na kuwakejeli
huku wakiimba kwa nguvu. Wachezaji wa Coastal Union walijibu mashambulizi kwa
kuwakejele ila mmoja wa wachezaji wa Azam alipishana kauli na mchezaji wa
Coastal hivyo wakaanza kurushiana mawe.
Zilizuka vurugu kubwa kiasi mchezaji wa Azam, Gadiel Michael
aliumizwa vibaya na kukimbizwa Hospitali. Hata hivyo viongozi wa michuano
waliingilia kati na kuwataka Coastal Union wasiondoe bus lao mpaka
atakapojulikana aliyempiga chuma mchezaji huyo.
Baada ya nusu saa polisi walifika uwanjani na kuwaita
viongozi wa timu zote mbili ndipo ilipobainika ni Yussuf Chuma ndiye aliyempiga
chuma mwenzake hivyo viongozi walimtaka kuomba radhi kwa mwenzake akiwa
Hospitali.
COASTAL UNION
14 JULAI, 2013
ARUSHA, TANZANIA
No comments:
Post a Comment