Hivi ndivyo vidume, Ally Kidi kocha msaidizi (aliyevaa kofia) na Hemed morocco kocha mkuu anayesalimiana na vijana. Hawa ndiwo watakaorudisha furaha ya soka jijini Tanga, taraa.
Mfungaji bora ligi kuu Zanizbar Abdallah Othman akishuka kwenye basi la timu. |
Wachezaji wa Coastal Union wakiwa katika uzi mpya kabla ya mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya URA.
Kwa utaratibu mpya aliouanzisha mwalimu Morocco bunduki hizi huanzia benchi, ila zikiingia timu inakuwa mpyaaa. Kutoka kushoto Selembe, Banda na Kibacha. |
MECHI kati ya Coastal Union na Simba SC imeonekana kuvuta hisia za wapenda soka wengi si tu Tanga na Dar es Salaam bali Tanzania nzima kutokana na timu hizo kuwa hasimu kwa kipindi hiki baada ya kuchukuliana wachezaji.
Timu hizo ambazo zinajifua na kujipima nguvu ili kuhakikisha wanashiriki ligi kuu msimu unaoanza mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, wakiwa vema kutimiza azma ya kutwaa ufalme wa soka Tanzania bara, watashuka dimbani leo saa kumi alasiri uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kwa mechi kubwa ya kirafiki.
Itakumbukwa ziara ya kanda ya ziwa kwa Simba haikutoa matokeo mazuri kutokana na kupoteza baadhi ya michezo huku mingine wakitoa suluhu, imewasili jijini Tanga jana jioni wakitokea Kigamboni kwenye ufukwe wa Bamba Beach walipojichimbia ili kujifua.
Coastal Union walioweka kambi Raskazone Hotel jijini Tanga, wao walianza vema mechi za kujipima nguvu kujiandaa na msimu ujao kwa kuwachapa wababe wa Simba, Uganda Revenue Authority kwa bao 1-0 wiki iliyopita kwenye uwanja wa nyumbani Mkwakwani.
Vyombo vingi vya habari vinaandika kuwa Simba wanawafuata wachezaji wao kiungo matata Haruna Moshi ‘Boban’ na beki hatari Juma Said ‘Nyosso’ lakini mashabiki wa Coastal Union wanasema hayo ni maneno ya mkosaji kwani wachezaji hao walionyesha dalili za kutupiwa virago na timu hiyo ndipo Wagosi walipoona umuhimu wao na kuwachukua.
Mbali ya hayo chipukizi aliyetokea Coastal Union, Ibrahim Twaha Shekuhe ambaye alisajiliwa na Simba mwishoni mwa msimu uliopita atacheza dhidi ya timu yake ya zamani kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na Simba.
Blog hii ilifanya mazungumzo na Ibrahim kujua anajisikiaje kupeleka mashambulizi katika timu yake ya nyumbani alisema, “Kwa kweli ndugu yangu Coastal Union ndiwo wanaonijua zaidi kuliko timu yoyote, haya ni maisha tu na kutafuta lakini kwasababu nimesajili Simba nitaichezea kwa moyo wote na leo nitacheza kama mshambuliaji wa Simba.”
Katika hatua nyingine kocha mkuu wa Simba, Abdallah Kibaden ana kazi kubwa ya kupanga timu yake kutokana na mkanganyiko uliopo kwenye timu hiyo juu ya wachezaji chipukizi na wachezaji wa zamani ambapo kombinesheni ya wachezaji hao imeonekana kushindwa hasa baada ya kuonekana chipukizi wanapocheza peke yao wanaonyesha uwezo mkubwa tofauti wanapochanganywa na wakongwe.
Mbali ya hayo Kibaden ana kazi ya kuwajaribu beki mpya Vincent Matsobane kutoka Black Leopards ya Afrika kusini, mwingine ni kiungo mkabaji wa zamani Azam FC, Abdulhalim Humoud ambaye ameibukia Simba akisaka nafasi ya kusajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Humoud aliyemaliza mkataba wake na Azam FC Mei, mwaka huu na kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa na klabu ya Jomo Cosmos, alionekana katika kambi ya Simba iliyokuwa, Kigamboni, Dar es Salaam.
Naye kocha wa Coastal Union, Hemed Morocco bado anasisitiza utaratibu wake mpya wa kuangalia mshambuliaji atakayemsaidia kufumania nyavu katika msimu mpya ili aweze kutimiza ndoto za watu wa Tanga kushangilia ufalme wa soka kwa mara nyingine tangu miaka 25 iliyopita.
Morocco ameahidi kuwaanzisha wachezaji wote wapya kama alivyofanya kwenye mechi dhidi ya URA ambapo mfumo huo ulimsaidia kuwapumzisha wachezaji wake tegemeo Abdi Banda, Suleiman ‘Selembe’ na mbwana Kibacha ambao kwa kiasi kikubwa walibadili mchezo wa siku hiyo mpaka likapatikana bao pekee lililokata ngebe za waganda waliozitambia timu kongwe nyingine.
COASTAL UNION
28 JULAI, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA
No comments:
Post a Comment