Haruna Moshi 'Boban' siku ya jana alizungumza kwa kujiamini sana hata kuwakosha mashabiki baada ya mchezo kuna kundi la watoto walimfuata wanataka kumgusa. Kwanza alitaka kukataa lakini akatokea Hussein Chuse akamwambia Boban watoto wanataka kukugusa, ndipo akakubali wacha wamparamie.
Hemed Morocco ni kwacha ndugu yangu maneno hayo yashikeni, anajua kumbadili mchezaji akacheza namba ambayo hajawahi kuicheza. Sasa yupo kwenye program ya kumchezesha Danny awe mshambuliaji wa kati.
Huyo aliyeruka juu ni Captain Jerry Santo taraa...
Mchezaji anapokuwa professional huwachwa afanye anachoamini.
Zipo dalili hawa viumbe wakawa super sub. Ni mawazo tu, kutokana na mfumo mpya wa mwalimu Morocco. |
Hapo Morocco anamwambia Abdi Banda kaa na mpira kaa na mpiraaa... Wataalamu wameshaelewa.
Hizi ni furaha za bao dakika ya 72 ukiwaangalia hao URA wamepagawaaaaa, wanashika viuno atiii.
Kocha wa URA (mwenye kofia) akifanya mahojiano na wanahabari kutoka Tanga mara baada ya timu yake kulala 1-0 Mkwakwani.
Huyo aliyelala chini ni Juma Nyosso aliumia vibaya sana kwenye bega baada ya mchezaji wa URA kumtegea mgongo na kumshika mkono wakati Nyosso akiwa juu. Nafasi yake ikachukuliwa na Pius Kisambale.
Hapo golikipa wa URA anawaambia mabeki wake, jamani mzuieni huyo anaitwa Odula mchezaji wa bei ghali amevuka maji kutoka Mombasa msimuacheeeee....
Zile salamu alizozizungumzia
mwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Hilal ‘Aurora’ kwa timu zinazoshiriki ligi
kuu zimetumwa rasmi jana kutoka uwanja wa Mkwakwani baada ya Wagosi wa Kaya
kuwatuliza 1-0 wababe wa Simba na Yanga, Uganda Revenue Authority waliokuja
Tanzania kujipima nguvu.
Pasi ya bao ilitoka
mguuni mwa beki wa kushoto Coastal Union, Abdi Banda katika dakika 72 ya mchezo
wakati wa kipindi cha pili walipokuwa wanashambulia kutoka lango maarufu la
African Sports, Banda alipofika usawa wa benchi la Coastal Union alilazimisha
kiki kali iliyotua katikati ya msitu wa wachezaji wa URA lakini mbali ya
wachezaji wa URA kulikuwepo na Mbwa mwitu (Keneth Masumbuko) aliyevaa ngozi ya
kondoo akaunasa mpira ule kwa mguu wa kushoto halafu bila kumtazama mtu alikunjuka
shuti kwa guu la kulia lililompunyua mikononi golikipa mahiri wa URA, Bwite
Brian aliyezidiwa ujanja na polisi huyo.
Ilikuwa ni
sawa na kesi ya nyani kumpa ngedere maana URA ni kikosi maalum cha kukusanya na
kudhibiti mapato nchini Uganda kama ambavyo TRA inafanya kazi Tanzania. Hivyo
Masumbuko yeye ametokea kwenye timu ya Polisi Morogoro yenye kazi ya kulinda
usalama wa raia hivyo ule upolisipolisi bado anao akahakikisha URA wanaondoka
nchini bila kuathiri usalama wa raia kwa kufungwa nchini mwao.
Mchezo
ulianza saa kumi na nusu alasiri baada ya mwamuzi wa siku hiyo Kidiwa kupuliza
kipyenga na wachezaji wa URA wakaanza kwa mashambulizi ya kushtukiza
yaliyowatia baridi mashabiki wa Coastal Union hasa ikizingatiwa dakika chache
siku hiyo kulinyesha mvua kubwa.
Mpaka
kufikia dakika ya 20 bado mchezo ulikuwa ni wa kuvuziana kwani timu zote mbili
zilikuwa zikisoma mbinu ya mwenzie ili kuhakikisha hawatoki kwa aibu kwenye
uwanja huo wa Mkwakwani unaochukua mashabiki 10,000.
Coastal
Union walikuwa wakishambulia kutoka upande wa kushoto ambapo combination ya
Uhuru Suleiman aliyekuwa akicheza namba 7 na Masumbuko Keneth ilimsaidia Danny
Lyanga ambaye siku hiyo alikuwa akishambulia kutoka kati tofauti na
ilivyozoeleka kocha akimchezesha winga ya kushoto.
Hata hivyo
juhudi hizo za kubadili mbinu za ushambuliaji hazikuzaa matunda zaidi ya
kuwazidisha ari mashabiki waliofurika kuangalia viwango vya wachezaji wapya
waliokuwa wakipamba magazeti kwa kipindi kirefu.
Nusu ya
kwanza mchezaji matata nje ya uwanja Haruna Moshi ‘Boban’ ndiye aliyekosha
mashabiki wengi kutokana na umahiri wake wa kumiliki mpira huku akipiga chenga
za maudhi na kutoa pasi za dhihaka utadhani anacheza na watoto wadogo lakini
pasi hizo zilifika miguuni mwa walengwa hali iliyowakosha wana mangushi.
Dakika 45
ziliisha bila kufungana, lakini kulitokea zengwe la sare za mchezo ambapo URA
walilalamika kuwa kuna mfanano wa aina fulani katika soxy na jezi za juu. Hivyo
kutokana na uenyeji kuchanganyika na ustaarabu ulikokuwepo Tanga Coastal Union
waliamua kubadili uzi wao mpya wenye rangi nyeupe tupu na rangi nyekundu
mabegani wakaamua kuvaa uzi mwekundu bila kujua rangi nyekundu ingekuwa na
bahati kwao siku hiyo.
Dakika 45 za
kipindi cha pili zilianza bila timu yoyote kufanya mabadiliko mpaka ilipofika 52 ambapo kocha Hemed Morocco alifanya
mabadiliko ya wachezaji watatu alitoka Hamad Juma, Danny Lyanga na Othman Tamim
akaingia Mbwana Kibacha, Suleiman Kassim ‘Selembe’ na Abdi Banda.
Kocha
akabadili mchezo ambapo Masumbuko sasa akawa anapiga krosi kutoka kushoto au
mara nyingine anamuachia Banda aliyekuwa akisaidiana na Uhuru apige huku yeye
anaingi katikati mwenyewe. Taktik hiyo ilizaa matunda dakika ya 72 ya mchezo
ambapo krosi ya Banda ndiyo iliyotua mguuni mwa Masumbuko na kupeleka kilio
jijini Kampala.
Baada ya
hapo Coastal Union wakawa wanalisakama lango la URA bila shaka kupata bao la
pili ili kujihakikishia ushindi.
Kufikia
dakika ya 85 almanusra URA wasawazishe baada ya Shaaban Kado kujaribiwa shuti
la mbali na kumponyoka kwa bahati nzuri liligonga mwamba wa juu na kutoka nje
ikawa kona. Ilipopigwa kona mpira ukambabatiza tena na kutaka kuingia lakini
akautoa tena ikawa kona pacha.
Vitendo hivi
vya dakika mbili viliwanyamazisha mashabiki 8000 wa Coastal Union waliohudhuria
na kuwapa nguvu mashabiki wachache wa URA waliokuwa kwenye benchi lao kutokana
na kuamini kuwa lolote linaweza kutokea. Kwa bahati nzuri kona ya pili haikuzaa
matunda.
Baada ya
hapo Wagosi wakaanza kucheza kiujanja ili kupoteza muda baada ya kugundua URA
wanaweza kuwachangua udhu kabla ya magharibi kuingia na futari ikawatumbukia
nyongo. Hatimaye mwamuzi akamaliza mpira yakatimia yale ya wazee kuwa mfupa
uliomshinda fisi mbwa kautafuna.
Kikosi cha
Coastal Union kilikuwa: Shaaban Kado, Hamad Juma, Othman Tamim, Marcus Ndehele,
Juma Nyosso, Jerry Santo, Uhuru Suleiman, Crispian Odula, Daniel Lyanga, Haruna
Moshi ‘Boban’, na Keneth Masumbuko. Akiba ni: Said Lubawa, Mbwana Kibacha, Abdi
Banda, Philip Mugenzi, Mohamed Sudi, Pius Kisambale, Suleiman Kassim ‘Selembe’,
Green Atupele na Abdallah Othman.
Baada ya
mechi kuisha mwandishi hakupata bahati ya kuzungumza na mwalimu Morocco maana alikuwa
anamvizia kocha wa URA, ambapo alipompata na kuzungumza mambo mengi kuhusu timu
yake na ziara ya Tanzania shukran katika mazungumzo yake hakugusia kuchoka kwa
timu yake ambapo makocha wa kibongo wengi hutumia kama kisingizio.
“Tanzania
kuna timu nzuri, hata mimi nimekuja kujaribu wachezaji wangu wapya wapo saba
kwa hivyo sikuwa na uchungu sana kupoteza mechi hii lakini timu tatu
nilizocheza nazo hapa nchini naziona zote zipo sawa.”
Akaulizwa
amecheza na Simba ameshinda 2-1, akacheza na Yanga akatoka suluhu ya 2-2 leo
amecheza na Coastal Union wamepoteza kwa bao 1-0 vipi maelezo yake. Akajibu: “The
answer is simple, timu iliyonifunga ndiyo best.”
COASTAL
UNION
25 JULAI,
2013
TANGA,
TANZANIA
No comments:
Post a Comment