Wapambanaji hawa walioiingiza timu nusu fainali. |
Manahodha wa timu zote mbili wakiwa na waamuzi wa leo. |
Furaha ya ushindi haina mipaka wala madoido. |
Kampeni ya kuchukua ubingwa wa michuano ya Rollingstone bila
kufungwa bao hata moja inazidi kukolea chumvi baada ya leo vijana wa Coastal
Union wagosi wa kaya kutinga hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa 1-0
walipokutana na Dareda FC jijini Arusha katika uwanja wa General Tyre.
Bao hilo lililoingizwa kimiani kwa mkwaju wa adhabu ndogo
baada ya mchungulia nyavu maarufu Ally Nassor ‘Ufudu’ kuchezewa madhambi nje
kidogo ya D hivyo nahodha msaidizi Ayoub Semtawa akapiga faulo iliyoingia
wavuni bila kipingamizi, hiyo ilikuwa ni dakika ya 64 kipindi cha pili.
Kipindi cha kwanza mambo yalikuwa magumu baada ya vuta
nikuvute ya dakika 45 kuisha bila timu yoyote kuchungulia wavu wa mwenzake;
lakini katika dakika ya 35 yuleyule bingwa wa mipira iliyokufa Ayoub Semtawa,
alikosa faulo iliyogonga mwamba huku golikipa wa Dareda FC kuruka upande
mwingine, wenyewe wanaita alimpeleka sokoni.
Kama kawaida yake Bakari Shime ‘Super Coach’ huwa anazitumia
vema zile dakika chache za mapumziko kwa kukipanga upya kikosi chake, ndivyo
alivyofanya leo baada ya kugundua ukuta wa Dareda haupitiki kwani Ally Ufudu
alikumbana na zahma nyingi kila alipojaribu kuingia na mpira.
Sifa kubwa ya Ufudu ni kasi na kumiliki mpira, walichofanya
mabeki wa Dareda ni kuharibu mipira anayopewa Ufudu ama kumchezea rafu mbaya,
hivyo kocha Shime akampanga Semtawa awe mpigaji faulo ama penati huku
akimsisitiza Ufudu kuendelea kukimbia na mipira bila kupiga mashuti ya mbali.
Ndipo ilipofika dakika ya 64 mbinu hiyo ikazaa matunda baada
ya Ufudu kuchezewa madhambi hatua chache kutoka eneo la kujidai la golikipa wa
Dareda. Kama kawaida Ayoub Semtawa aliutumbukiza kwa ufundi mkubwa mpira kasha Shime
akawataka wachezaji wake kubadilisha mbinu wazuie au kupaki bus.
Shime aliwatumia vema mabeki wake hatari Hamad Juma, Mwaita Saleh, Yusuf Chuma na
Nzara Ndaro ambao walijipatia majina kwenye michuano hiyo iliyofanyika mwaka jana
nchini Burundi na katika kombe la Uhai lililofanyika jijini Dar es Salaam,
ambapo katika michuano yote walifika hatua ya fainali na kutolewa kwa mikwaju
ya penalt. Burundi walitolewa na Ecofoot ya Congo wakati Dar es salaam
walitolewa na Azam FC ‘wana lambalamba’.
Mungu akipenda nusu fainali inachezwa kesho ambapo Coastal
Union wanasubiri mshindi wa mechi namba 25 ambao ni Simba SC na JKT Oljoro,
wanacheza leo asubuhi hii. Fainali itapigwa Julai 15 siku ya jumatatu.
Mungu ibariki Tanga, Mungu ibariki Coastal Union.
COASTAL UNION
12 Julai, 2013
No comments:
Post a Comment