Timu ya soka Coastal Union ‘Wagosi wa kaya’ kutoka Tanga
kesho itashuka dimbani kucheza pambano la kirafiki la kimataifa dhidi ya Uganda
Revenue Authority (URA) katika uwnaja wa Mkwakwani saa kumi alasiri.
URA kutoka Uganda waliokuja nchini kwa mechi za majaribio
kabla ya kuanza msimu mpya wa ligi nchini mwao tayari wameshacheza mechi mbili
kati ya Simba na Yanga.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Wagosi wa Kaya, Hemed Hilal ‘Aurora’
timu yake itacheza na URA ili kutuma salamu kwa timu nyingine zinazoshiriki
ligi kuu Tanzania bara kutokana na usajili kabambe walioufanya mwaka huu.
“Hii mechi si rahisi kama watu wengine wanavyodhani lakini
tumeamua kucheza na URA kama moja ya kampeni yetu ya kutuma salamu kwa timu
zinazoshiriki ligi kuu, maana Simba na Yanga wameshindwa kuwafunga hawa waganda
lakini sisi tutawafunga.
“Kauli mbiu ya timu yetu msimu ni ubingwa, mkumbuke hii ni
mechi ya kwanza kubwa tangu tumalize ligi kuu msimu uliopita, wachezaji wengi
ni wapya na bado hawajajuana vizuri lakini baada ya kuzungumza na kocha akasema
hana neno na kikosi chake kipo tayari kwa mechi, hivyo mashabiki wetu waje kwa
wingi kuangalia mechi hii ili hawa waganda wasijisifu kuwa wamekuja Tanzania na
hawajafungwa mechi hata moja,” alisema aurora.
Naye kocha mkuu wa Wagosi, Hemed Morocco amesema kikosi
chake ni kizuri ingawa bado mazoezi hayajawakolea kwani hawana muda mrefu tangu
waingie kambini, lakini anaamini watawapa furaha mashabiki wa Tanga kwa mechi
ya kesho.
Alipozungumzia suala la washambuliaji ambalo lilikuwa tatizo
msimu uliopita Morocco alisema, ‘Bado sijapata mshambuliaji, nimeangalia katika
timu nzima sijaridhika na safu ya ushambuliaji lakini hakuna kinachoshindikana
ligi inaanza msimu ujao hawahawa nilio nao nitawaelekeza namna ya kufanya maana
kazi ya kocha ni kumfundisha mchezaji kufanya asichokijua.”
Katika hatua nyingine Morocco alitoa ufafanuzi wake juu ya
upangwaji wa ratiba ya msimu unaoanza mwezi ujao kwa kusema hana tatizo na
ratiba.
“Sina matatizo sana na upangwaji ratiba huwa naamini ni
lazima tucheze mechi mbili, moja nyumbani na nyingine ugenini sasa hata iweje
ratiba lazima izunguke. Hata sisi Coastal Union hatuna tabu sana maana ratiba
inaonyesha katika mzunguko wa kwanza tunacheza mechi saba ugenini na sita
nyumbani ni kama nusu kwa nusu haina tabu tutacheza soka.”
Kwa upande wake nahodha msaidizi wa Wagosi Mbwana Kibacha,
amesema “Wachezaji wana morali ya juu sana ingawa hatuna muda mrefu tangu
tuingie kambini lakini katika mazoezi tunaelewana na hata juzi tulicheza mechi
ya wenyewe kwa wenyewe nadhani kocha ameridhika na kiwango tulichoonyesha.
“Kuhusu kuchelewa kuanza mazoezi sina tatizo sana maana
wachezaji wote walianza mazoezi wakiwa nyumbani, unajua mchezaji anayejitambua
huwa hakai kizembezembe hivyo wote wamekuja tayari wakiwa wameiva.”
URA tangu imekuja nchini imecheza mechi mbili dhidi ya Simba
jumamosi iliyopita ambapo Simba walilala kwa mabao 2-1, mechi nyingine
walicheza dhidi ya Yanga ambapo walitoka suluhu ya 2-2 ikiwa Coastal Union
watachapwa katika mechi ya kesho URA wataondoka Tanzania wakiwa kifua mbele
akini ikiwa watatulizwa basi Wagosi hao watapata sifa kubwa.
Aidha wachezaji wapya wa Coastal Union ni Haruna Moshi
'Boban', Juma Said 'Nyosso', Marcus Ndehele na golikipa Said Lubawa, kuna
mchezaji kutoka Jamhuri ya Pemba Abdullah Othman Ali, mwingine ni Kenneth
Masumbuko na Uhuru Suleiman aliyekwenda kwa mkopo kutoka Azam FC. Huku kutoka
Kenya wakinasa mchezaji mmoja wa Bandari Mombasa,
NB: blog ya Coastal Union inafanya taratibu za kuhakikisha itakuwepo
kwenye mechi ili kupata picha na matukio mbalimbali, lakini pia kwa wale
wafanyabiashara blog hii inafungua milango kutangaza nasi kwa bei nafuu ili
kuipa uwezo wa kusafiri na timu kila inapokwenda. Wasiliana nasi kwa namba +255
752 593894/ +255 713 593894.
COASTAL UNION
23, JULAI, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA
No comments:
Post a Comment