Hakika ilikuwa siku ya kupendeza kwa maana magari, pikipiki na baskeli zilijaa mtaa mzima wa 11.
Viongozi kwanza walikutana kujadili kuhusu suala lililoanza kusumbua vichwa vya wanachama, yaani wenye kadi ya uanachama waruhusiwe ama wasiruhusiwe kwenye mkutano.
Umewaona hawa, walichokuwa wakishikilia ni hilo gazeti la Mwananchi ambalo liliandika kila mwanachama ahudhurie awe na kadi ama asiwe na kadi. Ila baadaye viongozi walitumia hekima na kuamua kila mwenye uwezo wa kulipia siku hiyo basi afanye hivyo.
Kassim Siagi katibu wa Coastal Unio (mwenye sahti la mistari) akiwa na meneja wa timu Akida Machai wa kwanza kushoto pamoja na wanazi wengine wa timu wakiingia ukumbi wa mkutano siku ya jumapili. |
Mwenyekiti wa Coastal Union Hemed Hilal 'Aurora' akiwa nje ya ukumbi wa mkutano na wasaidizi wake.
Watoto hawa ndiwo watakaokuwa wanahistoria wa timu maana wameanza kufuatilia mwenendo wa timu mapema.
Pichani kutoka kulia unaonekana uso wa Tafa Boy, Hussein Chusse, Bawazir, Kiraka, Mwenyekiti Aurora na Ubinde.
Mkutano ukiwa umeanza na hapa wanachama wanaomba dua na kukumbuka waliotangulia mbele ya haki.
Pichani anaonekana Mzee Shossi (springit) wa kwanza kulia mwenye miwani ambaye alikuwa golikipa tishio wa Coastal Union, kilio chake kikubwa ni kusahauliwa kwa wazee wa timu, lakini mwenyekiti amemuahidi wataandaliwa utaratibu maalum wa kukumbukwa.
Mabingwa wa soka
Tanzania mwaka 1988 Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' kutoka mjini Tanga wamefanya
mkutano wao mkuu kwa mafanikio baada ya wanachama kukubaliana kitu kimoja tu ‘msimu
ujao ushindi lazima’.
Muda mwingi ulitumika
kusoma ripoti ya mapato na matumizi kwa msimu uliopita hasa vikiangaliwa
vipengele vya mafanikio na pale tuliposhindwa kutokana na matatizo ya fedha. Katibu
mkuu wa Wagosi wa Kaya Kassim Siagi, alipokuwa akitoa taarifa ya mapato na
matumizi kwenye mkutano huo uliofanyika jumapili June 30 ambao umevuta hisia za
mashabiki wengi wa klabu hiyo tangu miaka 1990 ilipokuwa ikiwika kwenye medani
ya soka, alisema wanachama hawana budi kuichangia klabu yao ili kutimiza
malengo ya kutwaa ubingwa msimu ujao.
"Mkumbuke leo
Juni 30, ndiyo tunakamilisha kalenda yetu ya mwaka hivyo jiandaeni kulipia ada
za uanachama ili kutunisha mfuko wa klabu kwani bila fedha za uhakika hatuwezi
kutimiza hata nusu ya ndoto zetu za kutwaa ubingwa msimu ujao.
"Msimu uliopita
tulitumia takriban mil 500, lakini vyanzo vya mapato havikufikia kiasi hicho
ada za uanachama, fedha za wadhamini wa ligi pamoja na mapato ya mlangoni
havikuzidi mil 300, mkumbuke klabu yetu haina mdhamini bali tuna wahisani
ikifika siku wakichoka hawa wahisani tutashindwa kuendesha klabu," alisema
Siagi.
Kwa upande wake meneja wa timu hiyo Akida Machai alihoji juu ya udhamini wa Simba Cement kwenye timu maana mbali ya kutoa basi dogo hakuna msaada mwingine wowote wanaoutoa kwenye timu mbali ya kuwatangazia bidhaa yao Tanzania na nje ya Tanzania.
Katibu alitoa majibu kuwa upo utaratibu unaofanywa kuangalia namna ya kuondoa nembo za kampuni hiyo ya Cement nchini Tanga, lakini ikiwa watakubali kuingia mkataba wa kuisaidia timu hiyo wataendelea kuziacha nembo za kampuni ya Cement. Lakini akaweka wazi kuwa mpaka sasa timu haina mdhamini zaidi ya wahisani u wanaoongozwa na kampuni ya betri za magari na matairi yaani Binslum Tyre.
Kwa mujibu wa
mkurugenzi wa ufundi Nassor Binslum, huenda kikosi kikaanza msimu wa ligi
Tanzania bara wakiwa na udhamini mnono kutoka kampuni kubwa ya vifaa vya
michezo, Umbro Ltd.
Akizungumza katika
mkutano huo uliofanyika klabuni barabara 11 mjini humo, mkurugenzi wa ufundi
Binslum, alisema tayari mazungumzo baina yao na kampuni ya Umbro yanafikia
ukingoni na huenda msimu unaotarajiwa kuanza mwisho wa mwezi huu wakavaa jezi
zilizotengenezwa na kampuni hiyo.
"Mazungumzo
yanafikia ukingoni na Umbro, ni kampuni kubwa ya vifaa vya michezo ndiwo
wanaowavalisha Manchester City na timu ya taifa ya Uingereza hivyo tunatarajia
msimu ujao kuvalishwa na Umbro kuanzia jezi, viatu, soxy, mipira, mabegi ya
kubebea vifaa vya mazoezi na nguo mpaka beji ya nahodha kwa kifupi kila kitu
cha mchezaji.
"Tumebakisha
kipengele kimoja tu cha maakubaliano kuhusu kununua jezi za mashabiki elfu
thalathini kwa bei ambayo wamepanga wao ingawa tunaiona kubwa lakini
hatutashindwa kufungua mazungumzoa tena ili mambo yaende sawa maana
wameshatutumia mfano wa jezi watakazotuvalisha, wanachosubiri ni jibu kutoka
kwetu kuwa wazitengeneze," alisema Binslum.
Baadhi ya wanachama
walisuguana sana juu ya uhalali wa katibu mkuu wa timu kuteua wanachama kwa
nafasi mbalimbali za kiutendaji, lakini hali ya hewa ilirejea baada ya
kunukuliwa vipengele katika katiba ya timu ambavyo vinaonyesha kumpa nafasi
katibu kuteua na hata kuajiri.
Katika hatua nyingine
wajumbe wawili wa kamati ya utendaji walipigiwa kura ya kutokuwa na imani nao
baada ya kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kiutendaji.
Naye mwenyekiti wa
klabu hiyo kongwe iliyoanzishwa mwaka 1948, Hemed Hilal 'Aurora' alisema kauli
mbiu ya mwaka huu ni 'Coastal Union bingwa' kwani awali walipokuwa wakitoa
kauli mbiu za kushika nafasi tatu za juu walikuwa wakijipima ikiwa wataweza
mikiki ya ligi kuu baada ya kukaa nje ya ligi kwa takriban muongo mmoja.
"Mtakumbuka huu
ni msimu wetu wa pili tangu turudi ligi kuu hivyo tayari tumejifunza mbinu
nyingi hasa ikizingatiwa miaka ya nyuma ligi haikuwa na ushindani mkubwa kama
ilivyo sasa, zamani ligi iliendeshwa bila kutumia gharama kubwa lakini sasa
bila pesa klabu si tu inashuka daraja lakini ianweza kufa kabisa na ndiyo maana
tunaweka wazi kuwa msimu huu kauli mbiu yetu ni 'Ubingwa' nadhani mmeona
usajili tulioufanya," aliweka wazi Aurora.
Coastal Union 'Wagosi
wa Kaya' ni miongoni mwa klabu zilizoanzisha ligi ya taifa na baadaye ligi kuu
mwaka 1965 ambapo klabu nyingine ni Sunderland sasa inaitwa Simba SC, Cosmo
Politan, Dar es Salaam Young Africans na African Sports ya Tanga. Mwaka 1988
ilikuwa na kikosi imara kilichoiletea heshima kubwa ya kuwa wafalme wa soka
Tanzania na kupeleka ushindani mkubwa katika michuano ya Afrika Mashariki.
Itakumbukwa kwa miaka
ya 1970-80 Coastal Union ilikuwa ni timu iliyoleta ushindani mkubwa katika soka
mpaka kuifanya Tanga kuwa mkoa wa pili wenye ushindani wa soka Tanzania baada
ya Dar es Salaam.
COASTAL UNION
1 Julai, 2013
TANGA, TANZANIA
No comments:
Post a Comment