Monday, July 8, 2013

Coastal Union yaipiga Young Life 3-0 Rollingstone Cup bUwanja wa General Tyre Arusha leo.

 Team Captain Nzara Ndaro kushoto akiwa na jembe lake Ally Nassor 'Ufudu' aliyepachika mabao mawili.

 Vijana wakikaza buti wakisubiri kuingia uwanjani kufanya mambo, hakika raha itakwenda Tanga mwaka huu.

Khalifan Mbaruku akiangalia namna uwanja ulivyo mkavu lakini lazima ucheze kupeleka heshima nyumbani.


Coastal Union chini ya miaka 20 imeanza vema harakati za kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana Rollingstone inayofanyka jijini Arusha katika uwanja wa General Tyre kwa kushinda mabao 3-0 dhidi ya Young  Life ya jijini humo.
Mchezaji Ally Nassor ‘Ufudu’ ndiye aliyepeleka shangwe jijini Tanga kwa kupachika mabao mawili peke yake na kutoa pasi ya bao la tatu huku Behewa Sembwana, akipachika bao moja baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Ufudu aliyekuwa mwiba kwa mabeki wa Young Life.
“Ally Ufudu aliwapangua viungo wa Young Life mpaka mabeki na kubaki yeye na golikipa kisha akapachika bao murua mnamo dakika 22 ya mchezo, bao hilo lilidumu mpaka mapumziko ambapo kama kawaida yake kocha mkuu wa Coastal Union B, Bakari Shime aliwapanga vijana wake kwa mawaidha  na kuwakosoa kidogo.
“Kipindi cha pili kilianza kwa mashambulizi ya kushtukiza kutoka kwa wapinzani wetu ambao walidhamiria kurudisha bao hilo, lakini golikipa wetu Idirisa alikuwa makini langoni mwake. Kufikia dakika ya 61 Behewa Sembwana, alipokea pasi maridhawa kutoka kwa Ally Ufudu akakimbia nao winga ya kulia na kupiga krosi iliyomshinda nguvu golikipa wa Young Life likawa ni bao la pili lililowamaliza nguvu wapinzani,” alieleza meneja wa timu B, Abdulrahman Mwinjuma ‘Ubinde’.
Aidha dakika nane kabla ya filimbi ya mwisho yaani dakika 82 yuleyule Ally Nassor ‘Ufudu’ aligongolea msumari wa mwisho kwenye jeneza la Young life huku mashabiki wachache wa Coastal Union wakiimba nyimbo za maombolezo kuashiria kifo cha ‘madogo janja’ hao waliozidiwa akili na vijana wa kipwani waliokwenda Arusha na chupa za kahawa wakiashiria hawana wasiwasi na ubingwa ni suala la muda tu.    
Kwa matokeo hayo Coastal Union wamejikusanyia point tatu wakisubiri mechi mbili kati ya JKT Oljoro na Testimonial Academy ili kuweza kujihakikishia kuingia hatua nyingine ya michuano ambapo  kesho watashuka dimbani dhidi ya maafande wa JKT Oljoro katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid saa kumi jioni na keshokutwa watacheza dhidi ya Testimonial Academy katika uwanja wa General Tyre saa tano asubuhi.
Michuano hii inashirikisha timu 16 za vijana ambapo kwa mwaka huu hakuna timu iliyotoka nje ya Tanzania hivyo Coastal Union inahitaji kuvuka hatua hii kwa hali na mali ili kujihakikishia ubingwa. Kundi la Coastal Union lina timu nne ambazo ni Coastal Union, JKT Oljoro, Young Life na Testimonial Academy.
Mungu ibariki Tanga, Mungu ibariki Coastal Union itwae kombe hili.
COASTAL UNION
Julai 8, 2013

Picha zote kwa hisani ya: mchezaji wa Simba Ibrahim Twaha Shekuhe, aliyekuwa Arusha.

No comments:

Post a Comment