Sunday, July 28, 2013

Coastal Union wazee wa dozi wamchinja mnyama Mkwakwani.

Coastal Union wakinyoosha viungo kabla huku kocha msaidizi ally Kidi akiwaangalia.
Vikosi vyote viwili kabla ya mchezo kuanza.

Hapa vijana wakishangilia bao pekee la leo lililotumbukizwa na Crispian Odula Odwenye.

Wagosi wa kaya wameendelea kutuma salamu kwa timu zinazoshiriki ligi kuu Tanzania bara kwa kuwachapa 1-0 Simba SC kwenye mechi ya kirafiki kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu ya Vodacom.
Mfungaji wa bao hilo ni mshambuliaji Mkenya, Crispian Odula aliyesajiliwa kutoka Bandari ya Mombasa.
Mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki wengi uwanja wa Mkwakwani, ilikuwa gumzo kwenye viunga vya mji wa Tanga na Dar es Salaam ambapo Simba waliingia jijini hapo wakijitapa kulipiza kisasi cha msimu uliopita baada ya kubaniwa kupata point za bure na kutoka suluhu.
Kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa kujihami huku kukiwa na mashambulizi ya kushtukiza ambapo mpaka dakika 45 za mwanzo hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.
Kipindi cha pili Coastal Union waliingia kwa kasi na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara kitu kilichompa wakati mgumu golikipa wa Simba, Mganda Abel Dhaira.
Kufikia dakika ya 54 Crispian Odula anayeheshimika sana ndani ya jiji hilo alipokea pasi safi kutoka kwa Keneth Masumbuko, akauacha udunde ndani ya eneo la hatari, akaja mchezaji wa Simba akampiga tobo akainua macho kumuangalia Mganda Dhaira akamekaa uelekeo gani, alipoona amekaa katikati ya lango akapiga kwenye nyavu ndogo na kuwatia wazimu mashabiki wa Coastal Union waliojaa ndani ya uwanjani utadhani hakuna Ramadhani.
Kitu kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu ni kuona kama mchezaji chipukizi aliyetoka Coastal Union, Ibrahim Twaha ‘Messi’ atacheza ama la, lakini kufika dakika ya 70 aliingizwa kuongeza mashambulizi baada ya Simba kuelemewa. lakini kocha Morocco alifanya ujanja kwa kumuingiza kijana mwenzie waliocheza pamoja timu B, Hamad Juma ‘Basmat’.
Kazi ya ‘Messi’ ikawa imeishia hapo kwani Hamad alipewa kazi moja tu ya kuhakikisha ‘Messi’ akifika winga ya kushoto ilipo ngome yake hapigi krosi. 
Mbwana Kibacha na Juma Nyosso wakaambiwa wahakikishe kijana huyo mwenye mbio nyingi havuki ukuta wa Coastal Union. Mwisho akaonekana hana msaada wowote kwa timu namna alivyodhibitiwa.
Kikosi cha Coastal Union: Shaaban Kado, Mbwana Kibacha, Othman Bakari, Juma Said ‘Nyosso’, Marcus Ndehele, Jerry Santo, Uhuru Suleiman, Crispian Odula, Keneth Masumbuko, Haruna Moshi ‘Boban’, na Daniel Lyanga.
Baadaye kocha mkuu wa coastal Union akishirikiana na Ally Kidi walifanya mabadiliko kwenye kipindi  cha pili kwa kuwatoa Uhuru Suleiman, Daniel Lyanga, Crispian Odula na Othman Bakar . Wakaingia Abdi Banda, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Mohammed Sudi na Hamad Juma ‘Basmat’.
COASTAL UNION
28 JULAI, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA


No comments:

Post a Comment