Na Hafidh Kido
Michuano ya Uhai Cup
iliyokuwa ikishirikisha vijana chini ya miaka 20 kwa timu zinazoshiriki ligi
kuu ya soka Tanzania
bara imekamilika rasmi jumapili tarehe 23, Desemba wiki iliyopita kwa Azam FC
kutawazwa mabingwa baada ya kuifunga Coastal Union kwa penalt 3-1 baada ya
dakika 120 kuisha kwa sare ya 2-2.
Hakika Rais wa shirikisho la
mpira wa miguu nchini TFF Leodger Tenga anastahili pongezi kwa kuanzisha
utaratibu wa kuweka sheria inazozibana timu zinazoshiriki ligi kuu kuwa na timu
ndogo za vijana wa chini ya miaka 20. Utaratibu huu lengo lake ni
kuibua vipaji vya vijana ambao awali walikuwa wakiishia kucheza timu za shule
na kubaki mitaani bila kuonekana katika dunia ya michezo.
Kanali Iddi Kipingu aliekuwa
mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Makongo ndie aliekuwa wa kwanza kusaidia
vijana kwa kuwachukua kutoka katika michuano ya shule za sekondari na msingi
maarufu UMISETA na UMITASHUMTA aliwaingiza katika shule yake halafu
anawasomesha bure huku akiwakuza vipaji vyao.
Utaratibu wake huu ulisaidia
kuibua vipaji vya wachezaji waliokuja kusumbua sana
katika soka la Tanzania ,
miongoni mwao ni kipa namba moja wa Taifa Stars Juma Kaseja, wachezaji wengine
hatari kama Bonifas Pawasa, Nico Nyagawa,
Renatus Njohole na Haruna Moshi ‘Boban’.
Lakini kwa sasa ni lazima kwa
timu yoyote ya ligi kuu kuwa na timu ya vijana, kama timu itakwenda kinyume na
utaratibu huu inaweza hata kuondolewa kwenye michuano; zamani timu kubwa tu
kama Simba na Yanga ndizo zilizokuwa na timu B ambapo walizitumia kuvuna
wachezaji wapya kwa matumizi ya baadae ingawa haikuwa lazima kufanya hivyo.
Coastal Union B ina miaka
mitatu tangu ianzishwe, nimekuwa nikifuatilia maendeleo yao
nimegundua ni timu yenye vijana wenye vipaji vya hali ya juu ingawa hawana
kambi rasmi ‘Academy’ kama wanavyofanya Azam FC, Simba SC na
Yanga ambazo ndizo timu zinazofanya vizuri katika ligi kuu ya bara.
Kudhihirisha hayo siku ya
fainali iliyowakutanisha Coastal Union kutoka Tanga na Azam FC ya jijini Dar es
Salaam, meneja wa Azam FC Said Salim Bakhresa ambae pia yupo katika kamati ya
maandalizi ya michuano hiyo, alipopata nafasi ya kusema chochote hakusita kukimwagia
sifa kikosi cha Coastl Union chini ya miaka 20 kuwa ni kikosi bora katika
michuano hiyo.
“Niwashukuru sana
sana tena sana
viongozi wa Coastal Union kwa kuweza kuwalea vijana hawa mpaka kuweza kucheza
soka katika kiwango cha juu kama hiki, hakika sikutegemea kama
wangeweza kucheza namna hii. Walistahili kushinda mchezo huu lakini bahati
haikuwa yao ila
nikiri tu Coastal Union chini ya miaka 20 ni timu nzuri ya vijana niliyowahi
kushuhudia hapa nchini,” Bakhresa.
Si hao tu hata Kanal mstaaf
Iddi Kipingu na Leodger Tenga kwa vipindi tofauti waliimwagia sifa Coastal
Union kwa kuweza kuwaandaa vijana wao na kuweza kutoa burudani ya hali ya juu.
Katika michuano hiyo Coastal
Union hawakupoteza mchezo hata mmoja katika michezo sita waliyocheza ambapo
minne katika makundi miwili ni ya robo na nusu fainali. Katika michezo yote
hiyo walionyesha soka la hali ya juu hasa katika robo fainali walipokutana na
Ruvu Shooting uwanja wa Chamanzi, mpaka wanakwenda mapumziko Coastal walikuwa
nyuma kwa magoli mawili.
Lakini waliporejea kwa
kipindi cha lala salama vijana wa Coastal Union walifanikiwa kurudisha magoli
yote mawili na kuingia hatua ya penalt ambapo walifanikiwa kusonga mbele baada
ya kushinda penalt 4-3. katika hatua ya nusu fainali walikutana na Simba SC
hiyo ndiyo mechi iliyokuwa ikiwasumbua kichwa, maana Simba walikuwa mabingwa
watetezi wa michuano hiyo na waliaminika kucheza soka la kuvutia.
Lakini hali ilikuwa tofauti
na vijana wa Simba walikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa vijana wa Coastal
Union hivyo kuvuliwa ubingwa rasmi na kuiwezesha Coastal Union kutinga fainali
ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Azam ndiyo iliyokuwa ya
kwanza kuingia fainali baada ya kuitoa Mtibwa Sugar kwa mikwaju ya penalt 3-2.
Ambapo matokeo ya dakika 90 za kawaida yalikuwa ni 1-1.
Katika fainali iliyokuwa
ikisubiriwa kwa hamu hasa ikizingatiwa Azam FC wanasifika kwa soka lao la
kuvutia ingawa mwaka huu waliingia dosari ya kuzomewa na mashabiki wakituhumiwa
kununua waamuzi lakini bado inabaki kuwa Azam ina wachezaji wenye vipaji na
wanalelewa kisoka huko katika kambi ya Chamanzi.
Katika kipindi cha kwanza
vijana wa Azam FC walionyesha soka hali ya juu kiasi kuwafanya viongozi wa TFF
na vyama vingine vya michezo kuwa kimya na kutoamini kilichokuwa kikitokea
baada ya kusikia kutoka kwa watu kuhusu kiwango cha hali ya juu cha vijana wa
Coastal Union ambao mpaka kipindi cha kwanza kinaisha walikuwa nyuma kwa mabao
mawili sifuri.
Hata hivyo katika kipindi cha
pili Coastal Union walirudi kwa kasi na kucheza soka la hali ya juu lililoamsha
kelele na kuwafanya viongozi wa soka kushindwa kukaa vitini kutokana na kiwango
kilichoonyeshwa uwanjani na Coastal Union .
Mpaka dakika 90 zinaisha
mabao yalikuwa 2-2, zikaongezwa dakika 30 lakini hali haikubadilika hivyo
kikaja kipindi cha mikwaju ya penalt na ndipo Azam FC walipotawazwa kuwa mabingwa
baada ya golikipa wao kuokoa mikwaju mitatu kutoka kwa vijana wa Coastal na
kushinda kwa penalt 3-1.
Mbali ya kombe bingwa wa
michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji ya Uhai
alipata kitita cha Tsh Milioni 1.5 wakati mshindi wa pili alipata kifuta jasho
cha Tsh Milioni moja.
Kitu ambacho kinanifanya
niendelee kuamini mpaka sasa kuwa Coastal Union walikuwa na kikosi bora timu yao ndiyo iliyotoa golikipa bora Mansour A. Mansour, kama hiyo haitoshi kocha wa Coastal Union Bakari Shime
ndie aliekuwa kocha bora wa michuano hiyo inayofanyika kila mwaka.
Aidha Ruvu Shooting imeibuka
timu yenye nidhamu, Ramadhan Mkipalamoto wa Simba ameibuka mfungaji bora kwa
kufunga mabao 6 na mchezaji bora ametokea Azam FC ambae ni Joseph Kimwaga, na
mwamuzi bora amekuwa ni Issck Mwalile..
Ushauri uliotolewa na Rais wa
TFF kwa viongozi wa Coastal Union ni kuhakikisha wanaitunza hazina hiyo ya
vipaji ambavyo kwa miaka ya baadae wanaweza kuiletea sifa Tanzania na Afrika kwa ujumla
katika usakataji kabumbu.
Mafanikio ya timu hii tangu
iundwe miaka mitatu iliyopita ni kushiriki mashindano manne ya vijana,
mashindano ya vilabu vya Afrika mashariki na kati kwa vijana chini ya miaka 20
yaani Rolling Stone walishiriki mara mbili, ambapo mara ya kwanza waliposhiriki
mwaka juzi waliishia hatua ya robo fainali mjini Arusha wakatolewa na wekundu
wa msimbazi Simba.
Mashindano ya mwaka huu ya
Rolling Stone yaliyofanyika mjini Bujumbura Burundi
vijana wa coastal Union walipata mafanikio makubwa hata kuweza kuingia fainali
wakafungwa na timu kutoka (Congo DRC), hivyo kushika nafasi ya pili.
Kombe la Uhai wameshiriki
mara mbili, mara ya kwanza kushiriki walitolewa katika hatua ya makundi, baadae
wakajipanga upya na mwaka huu wakaingiza tena timu kujaribu bahati. Ambao
walijaaliwa kushuhudia michuano ya Uhai mwaka huu watathibitisha maneno yangu
kuwa vijana walionyesha soka la hali ya juu hivyo kustahili kuingia fainali,
ingawa bahati haikuwa yao .
Si vibaya maana lengo la
michuano hii ya vijana si kuwa washindi kwa wakati wote, bali ni kuhakikisha
soka la vijana linakuwa kwa kasi na kuihakikishia nchi wachezaji wenye uwezo na
uzoefu wa kucheza soka mbele ya mashabiki wa nchi yoyote.
Si Coastal Union tu, bali
timu zote zinazoshiriki ligi kuu wanatakiwa kuwalea vizuri vijana wao ili
kuhakikisha maleno ya viongozi wa soka nchini yanatimia. Vijana ndiwo
watakaokuja kulikomboa soka la Tanzania .
DAR ES SALAAM , TANZANIA
costalunion@gmail.com
+255752 593894/ +255713
593894
2/1/2013
Mohammed Miraji aka Muddy magoli wa Coastal B ambae kwa sasa amepanda Coastal kubwa alipata kusifiwa na Rais wa TFF Leodger Tenga kuwa tangu aanze kuangalia soka la Tanzania kwa timu kubwa na ndogo hajaona mshambuliaji machachari kama huyu.... Kwanza mrefu na anajua kuutumia urefu wake na pili ana nguvu tatu ana uroho wa magoli, yaani akiona goli mate yanamjaa mdomoni kwa uchu.
Mansour akifanya mazoezi kabla ya mechi... huyu ndie kipa bora wa michuano ya Uhai U/20
Ally 'Ufudu' huyu akishangilia goli lake siku ya fainali dhidi ya Azam Fc
AAaahhggg Mtoto Messi huyooooo Ibrahim Shekue... nilitaka kujua kama ana udugu na Shekue Salehe.
Super Coach Bakari Shime aliweka historia kwa kufungwa kipindi cha kwanza na kurudi kisha kusawazisha, takriban michezo mitatu tofauti..
Super coach akipiga mafalaki...
Vijana wakiwa katika vyumba vya kubadili uwanja wa Chamazi katika game ya robo fainali Uhai Cup dhidi ya Ruvu Shooting.
Makamu mwenyekiti wa Simba Godfrey Nyange 'Kaburu' ambae ndie mlezi wa Simba B akimpongeza mwenyekiti wa Coastal Hemed Hilal 'Aurora' baada ya Coastal kuivua ubingwa Simba kwa mabao 2-1.
Hiki ndicho kikosi cha maangamizi Coastal U/20 taraa jamani.
No comments:
Post a Comment